1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMsumbiji

Rais Nyusi asema mji mwingine umevamiwa na wanamgambo

10 Mei 2024

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema jeshi la nchi hiyo linapambana na wanamgambo wa itikadi kali ambao wamefanya shambulizi kubwa leo, katika mji wa kaskazini wa Macomia.

https://p.dw.com/p/4fiiX
Jimbo la Cabo Delgado
Mashambulizi ya wanamgambo kaskazini mwa Msumbiji yamesababisha watu wengi kuyahama makaazi yaoPicha: ALFREDO ZUNIGA/AFP/Getty Images

Katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya Televisheni, Nyusi alisema kuwa makabiliano yalikuwa yakiendelea, lakini awali wanamgambo walikimbia baada ya kama dakika 45 za mapambano na kisha kurejea baada ya kujipanga upya.

Soma pia: Viongozi wa nchi za SADC kujadili masuala ya usalama mjini Lusaka

Shambulizi la Ijumaa linaonekana kuwa kubwa huku vyombo vya habari nchini humo vikiripoti kwamba limewahusisha wapiganaji wengi na raia wengi wamekimbia makazi yao.

Mji wa Macomia unapatikana katika jimbo la Cabo Delgado ambalo lina utajiri mkubwa wa gesi, ambako wanamgambo walio na mafungamno na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS walianzisha uasi mwaka 2017.

Licha ya kuwepo na juhudi kubwa za kiusalama za kushughulikia uasi huo, mashambulizi yameongezeka tangu Januari mwaka huu.